Mishamo Tz

Jumatano, 4 Oktoba 2017

Waziri Mkuu Apiga marufuku


Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amepiga marufuku kuwekwa ndani watumishi wa umma, wakiwemo wauguzi kwa tuhuma za kitaaluma.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa Pia, amewataka wauguzi kufanya kazi kwa weledi, uaminifu na kufuata maadili ya taaluma kwa kuwa maisha ya wagonjwa yako chini yao.

Waziri mkuu ametoa agizo hilo leo Jumatano akifungua mkutano mkuu wa 45 wa mwaka wa Chama cha Wauguzi Tanzania, mkoani Lindi.

“Naagiza viongozi wote kufuata na kuzingatia sheria. Kama kuna makosa ya kitaaluma, mabaraza husika yashughulikie jambo hilo na ni marufuku kuwaweka ndani watumishi kwa tuhuma za kitaaluma,” amekaririwa Majaliwa katika taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu leo Jumatano.

Awali, Naibu Waziri wa Afya,  Dk Hamisi Kigwangalla amesema baadhi ya viongozi wamekuwa wakiwakamata na kuwachukulia hatua watumishi wa sekta ya afya bila ya kufuata utaratibu jambo ambalo si sahihi.

Waziri mkuu amesema katika sekta ya afya bila wauguzi ambao ni kundi kubwa kati ya wanataaluma wa afya, Serikali haitaweza kutekeleza ipasavyo mikakati iliyopangwa kwa ajili ya kuiboresha.

Waziri mkuu amewaasa wauguzi kuhakikisha wanazingatia kiapo cha maadili ya kazi yao, akisema Serikali haitamvumilia yeyote atakayebainika kwenda kinyume.

“Nanyi wauguzi mna wajibu wa kutoa huduma kwa wananchi kwa kuzingatia kiapo na miiko ya taaluma yenu. Tunazo taarifa kuhusu baadhi ya wauguzi kutoa lugha chafu kwa wagonjwa, kuomba rushwa na wengine kujihusisha na vitendo vya wizi wa dawa,” amesema.

Majaliwa amesema lengo la Serikali ni kuhakikisha afya za Watanzania zinaimarika ili kuendana na kasi ya utendaji kazi wa Serikali ya kuinua uchumi na kufikia wa kiwango cha kati, hivyo ni lazima watoe huduma bora.

Amewaomba waunge mkono kwa nguvu zao zote jitihada za Serikali za kuhakikisha miundombinu na vifaa vyote havihujumiwi na watu wachache ili viwe msaada na hasa kwa wajawazito wajifungue salama.

Akizungumzia upungufu wa wauguzi nchini, Waziri Mkuu Majaliwa amesema Serikali itaendelea kuajiri watumishi wa kada mbalimbali wakiwemo wauguzi na wakunga na kuwapanga katika maeneo yenye upungufu zaidi.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni