Mishamo Tz

Jumapili, 1 Oktoba 2017

Mapishi ya piza ya mayai

=
Pizza ya mayai 

PIZA ni miongoni mwa vyakula vya kigeni, vilivyoingia nchini na kujizolea umaarufu.
Pamoja na uzuri wake, bado suala la upishi wa chakula hiki umekuwa ni  tatizo katika jamiii tofauti nchini.

Pizza asilia ni ile iliyobuniwa miaka kadhaa iliyopita nchini Italia. Lakini kwa kuwa mapishi ni sanaa, Wazanzibari nao hawakusita kubuni aina yao ya pizza.

Katika pizza asilia, jibini ndiyo kiungo kikuu kinacholeta upekee kwenye chakula hicho. Lakini katika upishi wa pizza ya Kizanzibari, mambo huwa ni tofauti kidogo, ambapo badala ya kutumia jibini, wabunifu hawa wa Kitanzania walienda mbali na kutumia ‘mayonize’ kama kiungo kikuu.
Je, ungependa kufahamu namna inavyopikwa?
Bila shaka ni ndiyo, hebu soma hapa;
Mahitaji

Unga wa ngano  nusu kilo
Mafuta ya maji
Maji kiasi
Vya kupambia pizza
Nyanya moja kubwa  iliyoiva vizuri
Kitunguu maji kikubwa
Mayonize
Mayai sita
Chumvi kiasi
Nyama ya kusaga iliyochemshwa na tangawizi
Namna ya kutengeneza
Chukua unga wa ngano na changanya na maji kidogo kidogo.
Hakikisha unalainika zaidi ya ule wa chapati na maandazi. Kata madonge madogo madogo ukubwa ndimu kubwa. Baada ya hapo anza kusukuma.

Sukuma kwenye kibao cha chapati hadi uenee katika kibao kizima. Baada ya hapo, chukua donge jingine, kisha kata nusu. Chukua hiyo nusu na kisha sukuma na weka katikakati ya duara lile la mwanzo.

Chukua nyama ya kusaga  kijiko kimoja na nusu kikubwa, chukua nyanya na vitunguu, katakata vipande vidogovidogo. Baada ya hapo chukua mchanganyiko huo, kisha weka juu ya lile duara la kati. Vunja yai moja, kisha weka kwenye mchanganyiko wako.

Chukua chumvi na nyunyizia kidogo, huku ukichanganya kwa kutumia kijiko. Chukua mayonize kijiko kimoja na changanya kwenye mchanganyiko wako. Kunja kuzunguka like duara la ndani na baada ya hapo kaanga kwenye chuma cha cha kukaangia chapati. Geuza geuza hadi pale itakapoiva kabisa.  Baada ya dakika tano pizza yako itakuwa tayari kwa kuliwa.

Ikiwa wewe ni mpenzi wa pilipili unaweza pia kula na pizza yako. Lakini ikiwa hupendei, siyo vibaya ukatumia sosi ya nyanya.

Imeandaliwa na Chef Mishamo Tz
Email:Mishamososthenes@gmail.com

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni