Mishamo Tz

Jumapili, 1 Oktoba 2017

Polepole: CHADEMA ruksa kufanya Mikutano Ikulu

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) pamoja na vyama vingine vyote vya upinzani nchini vimekaribishwa Ikulu kwenda kufanya mikutano yao kama vinataka.

Hayo yamesemwa na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Humphrey Polepole alipokuwa akijibu swali lwa mwandishi wa habari aliyetaka kujua kwanini CCM wanafanyia vikao vya chama Ikulu.

Mwandishi huyo wa habari alishangazwa na kitendo cha Meya wa Manispaa ya Ubungo, Boniface Jacob (CHADEMA) kuhojiwa kwa kosa la kufanyika kikao cha chama katika ofisi za Manispaa, lakini viongozi wa CCM wakaachwa  licha ya kuwa wamefanyika vikao vyao Ikulu ambayo si ofisi ya chama bali ni ya umma.

Akijibu swali hilo Polepole alisema kuwa, kwanza Meya sio mmiliki wa mali za manispaa na kwamba yeye katika manispaa anayo ofisi kama watumishi wengine na kwamba anatakiwa kwenda hapo kwa siku chache tu kama inavyoelezwa na sheria.

“Meya si mwenye manispaa, Meya si mmiliki wa mali za manispaa. Meya ana ofisi tu kwenye manispaa ambayo anatakiwa akae mle kwa siku kadhaa, sio muda wote, hivyo ni makosa kwa Meya kutumia mali za manispaa kwa matumizi yake binafsi,” alisema Polepole.

Polepole aliendelea kusema kuwa, Meya anatakiwa kutumia gari la ofisi kwa siku zilizoelezwa kisheria lakini pia kwa kazi ambazo zimeanishwa bayana, hivyo kuitisha vikao binafsi katika ofisi za manispaa za serikali ambayo iko chini ya dhamana ya Mkurugenzi ni kosa.

Polepole alisema kwamba Meya hawezi kutumia ukumbi wa Manispaa kwa sababu mwenye dhamana ya ukumbi huo ni Mkurugenzi wa Manispaa husika.

Akieleza kwanini ni halali kwa Rais ambaye pia ni mwenyekiti wa chama kufanyia vikao vya chama Ikulu, Polepole alisema, tulimachagua mtu mmoja tu Tanzania nzima na kumpa dhamana ya kuwa Rais Mtendaji wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

“Tumempa ofisi yake, Ikulu, tukampa nyumba Ikulu, wageni wake asiwaalike Ikulu,! wakazungumze!” alihoji Polepole.

Ikulu ndipo mahala Rais anapoishi, ndipo pahala usalama wake unakuwa imara zaidi.

Aidha, Polepole amesema kuwa Rais ambaye Ikulu ndipo makazi yake yalipo, hajasema vyama vingine haviwezi kwenye kufanyia vikao vya kule, na badala yake vinakaribishwa na viombe kwa kufuata taratibu ili vipatiwe kumbi za kufanya hivyo.

“Rais ambaye ndiye ana dhamana ya Ikulu hajasema vyama vingine visiombe kufanya mikutano Ikulu. Hivyo kama kuna vyama vimeguswa vinataka kufanyia mikutano yao Ikulu, nashauri vifuate taratibu za kuomba kutumia ukumbi wa ikulu kufanya mikutano yao,” alifafanua Polepole.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni