JINSI YA KUPIKA VIAZI VYA NYAMA VYA NAZI(STYLE 2)
Miongoni mwa vyakula vinavyonidondosha mate na kunifanya nile mpaka nivimbiwe ni viazi vya nazi. Ninapoulizwa nyumbani ni chakula gani tupike basi viazi vya nazi havikosekani kwenye orodha. Naam! Viazi vya nazi ni chakula maarufu mno Mombasa na kote pwani Kwa ujumla. Vile vile ni chakula ambacho kwamba ni nadra sana kukosekana wakati wa ramadhani. Pengine huenda kisipikwe mwaka mzima lakini Ramadhani ni lazima kitapikwa japo siku chache. Hili ni dhihirisho kuwa ni chakula kinachoenziwa na wengi. Bila shaka kama hukifahamu chakula hiki basi una hamu kuu ya kujua kinavyoandiliwa. Ungana nami tujifunze Kwa pamoja! Kumbuka! Raha ya viazi vya nazi ni vikolee nazi.
MAHITAJI
viazi kilo 1 vilivyochambuliwa maganda na kukatwa Kwa slices (hakikisha slices si nyembamba sana ili viazi visivurugike)
Nyama 1/2 kilo iliochemshwa na Chumvi (usiiache na supu nyingi kwasababu kuna matusha)
Tomato 2
Kitunguu maji 1
Pilipili boga/hoho 1
Dania 1
Kitunguu thomu kilichosagwa kijiko 1 cha mezani
Curry powder kijiko 1 cha mezani
Matusha(tui jepesi) vikombe 3
Tui zito kikombe 1
Chumvi kiasi
MATAYARISHO
Weka viazi kwenye sufuria kisha ukatie Katia ndani yake tomato, Kitunguu maji,pilipili boga na dania
Weka Kitunguu thomu, currypowder, chumvi na matusha ufunike viazi vyako viendelee kuiva Kwa moto wa kiasi
Kama viazi bado vigumu utaongeza matusha kidogo(hakikisha umeweka matusha ya akiba pembeni)
Viazi vikielekea kuiva weka nyama(kama nyama ni ngumu Sana unaweza ukaiweka mwanzoni wakati ukiweka tomato na vengivyengi)
Viazi vikishaiva, weka tui zito(unaweza ukaweka royco ukakorogea ukipenda)
Acha itokote Kwa dakika 3 na viazi vipo tayari
Andaa Kwa pilipili ya ndimu
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni