Mishamo Tz

Jumatano, 21 Septemba 2022

JINSI YA KUPIKA VIAZI VYA NYAMA VYA NAZI

​JINSI YA KUPIKA VIAZI VYA NYAMA VYA NAZI(STYLE 2)


 



Miongoni mwa vyakula vinavyonidondosha mate na kunifanya nile mpaka nivimbiwe ni viazi vya nazi. Ninapoulizwa nyumbani ni chakula gani tupike basi viazi vya nazi havikosekani kwenye orodha. Naam! Viazi vya nazi ni chakula maarufu mno Mombasa na kote pwani Kwa ujumla. Vile vile ni chakula ambacho kwamba ni nadra sana kukosekana wakati wa ramadhani.  Pengine huenda kisipikwe mwaka mzima lakini Ramadhani ni lazima kitapikwa japo siku chache. Hili ni dhihirisho kuwa ni chakula kinachoenziwa na wengi. Bila shaka kama hukifahamu chakula hiki basi una hamu kuu ya kujua kinavyoandiliwa. Ungana nami tujifunze Kwa pamoja! Kumbuka! Raha ya viazi vya nazi ni vikolee nazi.


MAHITAJI


viazi kilo 1 vilivyochambuliwa maganda na kukatwa Kwa slices (hakikisha slices si nyembamba sana ili viazi visivurugike)

Nyama 1/2 kilo iliochemshwa na Chumvi (usiiache na supu nyingi kwasababu kuna matusha)

Tomato 2

Kitunguu maji 1

Pilipili boga/hoho 1

Dania 1

Kitunguu thomu kilichosagwa kijiko 1 cha mezani

Curry powder kijiko 1 cha mezani

Matusha(tui jepesi) vikombe 3

Tui zito kikombe 1

Chumvi kiasi


MATAYARISHO


Weka viazi kwenye sufuria kisha ukatie Katia ndani yake tomato,  Kitunguu maji,pilipili  boga na dania

Weka Kitunguu thomu, currypowder, chumvi na matusha ufunike viazi vyako viendelee kuiva Kwa moto wa kiasi

Kama viazi bado vigumu utaongeza matusha kidogo(hakikisha umeweka matusha ya akiba pembeni)

Viazi vikielekea kuiva weka nyama(kama nyama ni ngumu Sana unaweza ukaiweka mwanzoni wakati ukiweka tomato na vengivyengi)

Viazi vikishaiva, weka tui zito(unaweza ukaweka royco  ukakorogea ukipenda)

Acha itokote Kwa dakika 3 na viazi vipo tayari

Andaa Kwa pilipili ya ndimu